Serikali
imetoa wiki moja kwa Mamlaka ya Usimamisi wa Bandari(TPA) mkoa wa Tanga
kuhakikisha inarejesha tena matumizi ya mita ya kupimia mafuta (Flow
Meters), kabla ya shehena ya meli ya mafuta kutia nanga bandarini hapo.
Hatua
hiyo ya serikali inafuatia uamuzi wa TPA kuacha ufungaji wa mita hizo
uliofanywa zaidi ya miaka mitano iliyopita ambapo kwa kipindi chote
hicho serikali ilikuwa ikiingia hasara na kupoteza mapato.
Hayo
yalibainishwa jana na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Mhandisi, Edwin Ngonyani wakati akizungumza katika majumuisho ya ziara
yake ya kikazi ya siku moja iliyolenga kuangalia mwenendo wa utendaji wa
Bandari ya Tanga.
Katika
ziara hiyo, pia Naibu Waziri alifanya ukaguzi wa Flow meters pamoja na
matishari matatu ambayo yamedumu kwa zaidi ya miaka minne bila kufanya
kazi bandarini hapo.
Mhandisi
Ngonyani alisema serikali imesikia kwamba kufungwa kwa mita za kupimia
mafuta(Flow Meters)kwenye bandari za hapa nchini kumetokana na ushiriki
wa baadhi ya wafanyakazi wa TPA waliokuwa wamelenga kunufaika kupitia
wafanyabiashara wakubwa ambao kimsingi mita hizo zilikuwa zikiwabana
katika ulipaji wa kodi.
Pia
imeelezwa kuwa baadhi ya wafanyakazi hao wanajihusisha kufanya
uchochezi kwa wananchi ambao walitakiwa kupisha maeneo yao kwa ajili ya
ujenzi wa bandari ya Mwambani, ambao licha ya kulipwa fidia lakini
wameendelea kugoma kuachia ardhi hiyo.
“Uamuzi
wa kuondoa Flow meters ulikuwa ni wa kipuuzi kabisa na tumesikia
uchochezi huu pia ulihusisha baadhi ya wafanyakazi," alisema Ngonyani.
"Inasikitisha sana kwani nia yao ilikuwa ni kuwanufaisha
wafanyabiashara."
Alisema
iwapo watumishi wa TPA wangekuwa na umoja katika kupigia kelele maamuzi
yaliyofanywa kipindi hicho, ni dhahiri kuwa hali ya ukwepaji wa kodi
kwenye shehena ya mafuta yanayoingia nchini isingefikia ilivyo sasa.
Alisisitiza
kwamba serikali itawachukulia hatua za kisheria waliohusika na manunuzi
ya matishari matatu kwenye Bandari ya Tanga ambayo hayakidhi vigezo vya
kiutendaji.
Aidha,
aliitaka Menejimenti ya mamlaka hiyo kupitia upya mkataba wa mzabuni
aliyeagiza vifaa hivyo kuona kama wataweza kunusuru kiasi cha fedha
zilizotumika.
“Kuna
haja ya kuupitia upya mkataba wa mzabuni tuone kama kuna njia yoyote ya
kuokoa zile fedha lakini bado tuendelee pia kuangalia namna ya haya
matishari yatakavyotumika kwa njia mbadala.
"Kama alivyosema Waziri Mkuu (juzi) nasisitiza kwamba aliyehusika tutamshughulikia.”
Mhandisi
Ngonyani alisisitiza kuwa wananchi wajenge imani na serikali ya awamu
ya tano kwamba Bandari mpya ya Mwambani itajengwa na kamwe haitakuwa
ndoto; hatua itakayoenda sambamba na ujenzi wa njia ya reli kutoka Tanga
mpaka Musoma.
Awali,
Kaimu Meneja wa TPA Mkoa wa Tanga, Kapteni Andrew Matillya alisema kwa
wastani wa kila mwezi Meli ya moja ya shehena ya mafuta inapukuliwa
bandarini hapo na kwamba utaratibu unaotumika kupima mafuta hayo si wa
flow meters kwani ziliondolewa tangu mwaka 2011.
“Kila
mwezi kuna wastani wa meli moja inapakua mafuta kwenye bandari hii
lakini utaratibu unaotumika ni wa bye-pass kwa maana kwamba flow meters
hazitumiki kupima kiasi cha mafuta kinachoingia nchini,” alisema.
Naye
Mbunge wa Jimbo la Tanga, Mussa Mbaruku (CUF), aliishukuru serikali ya
awamu ya tano kwa hatua mbalimbali inazochukua kama kurudisha matumizi
ya Flow meters na ahadi ya ujenzi wa bandari ya Mwambani.
Alisema maamuzi hayo yanajenga matumaini mapya kwa wananchi wa Tanga ambao walishakata tamaa.
Hivi
karibuni Serikali ilimsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo
nchini (WMA), Magdalena Chuwa na Meneja Vipimo Kitengo cha Bandari,
Bernadina Mwijarubi.
Mwijarubi ndiye anashughulikia kitengo cha mafuta bandarini.

No comments:
Post a Comment