Niwe Mkweli Kuhusu Richard Kasesela..
Ndugu zangu,
Jana nilifika kata ya Mlenge, Pawaga mapema asubuhi. Niliongea na
viongozi na wananchi walioathirika na mafuriko. Nilikuwa Mlenge saa tatu
kabla ya Richard Kasesela hajafika.
Viongozi akiwamo Mtendaji Kata waliniambia DC Kasesela wamekuwa nae kila siku tangu mafuriko yatokee.
" Mheshimiwa DC anashinda na sisi kila siku kuanzia asubuhi mpaka jioni.
Jana kaondoka saa kumi na mbili jioni." Anasema Sarah Mbilinyi,
Mtendaji Kata ya Mlenge iliyoathiriwa sana na mafuriko.
Nikafika kijijini Kisinga kuliko na kambi ya wahanga wa mafuriko
wanaotokea kitongoji cha Kilala kilichosombwa na mafuriko. Waathirika,
wakiwamo akina mama na watoto wanamzungumzia vizuri Richard Kasesela
wanayefyeka nae mapori na kujenga miundo mbinu mipya ya kitongoji cha
Kilala Mpya ambao kuna wanaotaka kiitwe Kitongoji cha Kasesela.
Nikiwa hapo Kisinga, na ilipofika saa tano asubuhi nilimwona Richard
Kasesela akiingia kambini hapo akiwa amevalia jeans, fulana na viatu vya
raba.
Viongozi wa kijiji na wahanga walionekana kuwa karibu nae sana. Watoto
wa hapo kambini walifurahia pia uwepo wake. Mara kadhaa alikatishwa
kwenye mazungumzo kutokana na viongozi wa kitongoji, wahanga na watoto
waliotaka kuongea nae.
Mimi siamini kabisa, kuwa Richard Kasesela anayafanya yale ya kule
Mlenge kwa wahanga wa mafuriko na kwingineko kwa sababu ya kulinda U-DC
wake. Nayaona akiyafanya kutoka kwenye moyo wake. Ni kiongozi wa
kupigiwa mfano.
Nimetaka kuusema ukweli wangu kuhusu Richard Kasesela, kwa ninavyooamini mimi, basi.
Maggid,
Iringa

No comments:
Post a Comment