ACT-Wazalendo
TAARIFA KWA UMMA:
Tumekuwa tukipokea simu za waandishi mbali mbali baada ya kauli ya jana
ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC),Jecha Salum Jecha kuwa
hakuna chama kilichojitoa katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika machi
20 mwaka huu
Msimamo wa ACT-Wazalendo ni kuwa hatutashiriki Uchaguzi huo kama
ilivyoazimiwa katika kikao cha kamati kuu cha february 14 mwaka huu
Hatushiriki kwa kuwa tunaamini kuwa hakuna sababu ya kufanyika uchaguzi mwingine nje ya ule uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana
Taarifa hii ya kutoshiriki uchaguzi wa machi 20 mwaka huu imewasilishwa
katika ofisi ya ZEC Zanzibar february 9 mwaka huu baada ya wao kututaka
tuthibitishe kwa maandishi kama tutashiriki au la
Hivyo kauli ya Jecha kuwa hakuna chama kilichofuata utaratibu ni
muendelezo mwingine wa kutaka kuhalalisha haramu kuwa halali kama
walivyofanya katika kufuta uchaguzi wa Oktoba 25
Kwa kuthibitisha dhamira yetu hii ya kutoshiriki hivi karibuni kamati
Maalum ya uongozi Zanzibar ilimsimamisha uanachama ndugu Khamis Idi
Lila,aliyedhaminiwa na chama kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar katika
uchaguzi uliofutwa kwa "Zengwe" hivyo hatuna mwanachama anayewania
nafasi hiyo
Jecha amezungumzia Sheria ya Uchaguzi na wajibu wa mgombea
aliyedhaminiwa na chama kuthibitisha ushiriki wake,huku akiacha kwa
makusudi kuainisha udhamini huo ni katika uchaguzi gani
ACT-Wazalendo haijamdhamini mwanachama wake yeyote kwa ajili ya
kushiriki uchaguzi wa Machi 20 na hili lilipewa msisitizo katika kikao
cha kamati kuu iliyofanyika february 14 na taarifa kutolewa kwa umma
siku iliyofuata
Tunaomba wananchi wapuuze ulazimishaji huu wa ZEC kwa kutaka kuionesha dunia kuwa vyama vimeshiriki uchaguzi huo haramu
ACT wazalendo katika kikao chake cha kamati kuu iliazimia kuwa haitakuwa
muhuri wa kuwasafisha wabakaji wa Demokrasia kwa kushiriki uchaguzi wa
Machi 20
Abdallah Khamis
Afisa Habari
ACT Wazalendo

No comments:
Post a Comment